The Chant of Savant

Saturday 1 April 2017

Dingi anapowachanganya walevi na kuchanganyikiwa

       Juzi nikiwa zangu kwenye misele si nikajikuta kwenye ufunguzi wa barabara za ghorafa kwenye kaya ambayo si baraba kiuongozi ukiachia mbali kuwa fiti kiuongo. Tokana na kutaka kujua nini majaliwa si yule dingi msaidizi namba mbili, ya walevi na kaya yao, si nikajikuta nikisikiliza mipasho ya dingi kwa mashakunaku na mashambenga wanaotaka amtoe mwanae wa pekee ili wamsulubu. Hawajui kuwa baba yuko ndani ya mwana na mwana yuko ndani ya baba na afanyacho mwana amefanya baba. Hamkuona juzi munene wa umbea alivyofurushwa kwa kutaka kumchunguza mwana?
            Dingi akiwa amepania si akaanza mipasho kama ya wale waimba twaarabu japo si waarabu! Kwanza, aliotongoa kuwa kuhusu maendeleo ya barabara ghorofa na ushamba wa walevi. Nilidhani hii ndiyo inshu iliyokuwa imemleta pale. Sikujua nilikuwa nimenoa kama yeye! Si akaanza kurusha mipasho na michemsho kwa wana mitandao na mitindio bila kuwasaza wale wabaya wanaomsakama mwanae kipenzi mwenye jina kama la mtume Po! Huku walevi waliokuwa wakisema mara amsulubu au kumtumbua si wakaisha kutumbikia nyongo kwa kukosa utumbuzi! Dingi bila kujali kuwa yuko pale kwa kura za kula za walevi akila na kusaza si aliwazodoa kuwa yeye hababaishwi wala kuingiliwa! Aliendelea kuchonga ‘ukiniingilia ujue umekwama.’ Sitakusikiliza. ‘mimi ni dingi anayejiamini hata pasipohitaji kujiamini kama kukingia kifua ufisadi na utapeli kama ule alioshitakiwa nao mwana wa Bashit, washit sorry Bashite. Badala ya dingi kuzima moto si aliukoleza mafuta huku akiwakwaza wateule wake wanaoshughulikia na umbea waliokuwa wameunda tume ya kuchunguza maovu ya mwana wa pekee.
            kama haitoshi, dingi aligoma kutumbua kile akipendacho. Badala yake alifoka na kuahidi kuwapuuza wale wanaomzonga mwanae kipenzi. Tokana na imani yangu ya uongo kuwa kaya yetu ni ya haki na usawa, si niliishia kuchefuka kiasi cha kutapika! Kipindi kile tulipofungwa kamba na kuwekwa sawa kuwa mambo ya kulindana na kubebana yalikuwa historia, si niliishia kujishangaa kwanini nilipoteza kura yangu. Nikiwa nimechanganyikiwa nisiamini niliyokuwa nikishuhudia si bongo akatunanga walevi kuwa tunapenda udaku. Hasira zilinipanda kiasi cha kumkumbuka bunga na kidhabi mmoja limbukeni aliyetunanga kuwa sisi tulikuwa wavivu wa kufikiri asijue alikuwa kiongozi wetu katika jinai hii aliyotuzushia. Jiulize; hata muulize. Aliishia wapi pale alipoweka na Dalila kishawishini akatuuza na kutuchuuza bila kujisaza. Ama kweli wakati mwingine ulevi wa maulaji ni hatari kuliko wa kanywaji. Nani alijua kuwa kinda lingejisahau wakati mabaya yake yanajulikana?
             Baada ya dingi kurusha makombora yake nilianza kumuonea huruma yule kidhabi na tapeli mwingine aliyekuwa akimhubiri mwana wa pekee asijue lao moja. Yule jamaa mwenye jina sawa na la paka Jimmy nadhani atakuwa ameumia na kuumbuka kama wale mashambenga. Maana, jamaa badala ya kuhubiri injili ya ufufuko na uzima, alihubiri ile ya visa, visasi na maangamizi asijue dingi atamstukia na kumtupia makombora ambayo bila shaka yamemmaliza. Je jamaa naye anaogopa nini kama hauzi bwimbwi? Au ni ile mimali isiyo na maelezo aliyowapora kondoo wajinga wa kaya ya walevi. Naona akae mkao wa kuliwa kama si kutumbuliwa.
            Hakuna kilichonitia aibu kama dingi kujiingiza kwenye siasa za chumbani mbele ya dingi wa kimataifa tena wa mshiko na njuluku. Sijui  kama ana washauri. Na kama anao sijui kama wanamshauri au anawapuuzia. Kama anawapuuzia si waachie ngazi badala ya kujidhalilisha kama wale viranja wake aliowaaibishia kwa kupinga amri zao. Ama kweli, heri kulewa kanywaji kuliko ulaji. Sijui hapa aliyelewa kati ya mashambenga na mashankupe wanaomkamia mwana wa pekee wa dingi kipenzi, dingi mwenyewe na mwana mwenyewe. Katika ulevi na ujinga wangu nilichanganyikiwa baada ya dingi kunichanganya, kujichanganya na kuchanganya kaya nikadhani ndoa ya baba na mwana ingevunjiliwa mbali nisijue kuwa si hivyo. Sasa tazama mwana tena chizi kapewa rungu. Je wanyonge tutapona? Waulize wale wa runinga na radio ya mawingu aliowavamia na kutia kashkash hadi wakahama mawimbini kwa siku mbili. Hapa sijui anayetawala na kutawaliwa ni nani kati ya baba na mwana. Sijui anayemtumia mwenzake kati ya wawili hawa ambao uwili wao unatisha ukiachia mbali kuwa zaidi ya utatu mtakatifu. Sijui huu niuite uwili mtakachafu au uwili mchanganyikiwa.
            Du, bangi, gongo na usingizi vitu vibaya. Kumbe naota! Kama si hivyo, nani alijua kuwa mhalifu tena aliyechapia na kukimbia umande angekingiwa kifua hiki ambapo akina Keinerugaba wanawagalagaza akina Makorongo Muhanga waliojiita madaktari wakati ni waganganjaa na matapeli. Ama kweli mwenye mapenzi haoni! Inakuwaje vitu simpo na vya wazi vinawapiga chenga madaktari? Inakuwaje kihiyo na kishite anamtapeli hadi kumlazimisha msomi kutia heshima na ulaji wake kitanzini? Ama kweli, ukishangaa ya Njaa Kaya utaona ya Kanywaji! Nani alijua kuwa kaya yetu ingeendelea kuwa gamba na chaka la matapeli na mafisadi wa elimu ukiachia mbali walevi wa madaraka? Ama kweli hii ni kaya ya walevi au Bongolalaland aka Danganyika. Vinginevyo ningewaona walevi na michupa yao wakienda kusafisha ofisi zao kwa kuwaponda wachafu waliojazana huku wakiwaburuza na kuwatukana kuwa ni wadaku mchana kutwa.
Kumbe naota!
Chanzo: Nipashe Jumamosi leo. 

No comments: