The Chant of Savant

Wednesday 7 June 2017

Barua Ya Wazi Kwa IGP Sirro

Image result for photos of igp sirro
            Kamanda Sirro,
Kwanza nakupongeza kwa kuaminiwa na kuteuliwa kuwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP). Pia, kukupa pole kwa kurithi mizigo na madudu kibao kuanzia mauaji ya Kibiti, kukithiri kwa rushwa kwenye jeshi lako, mishahara midogo, matumizi mabaya ya jeshi husika ambalo limekuwa likitumika kisiasa zaidi ya kiusalama.
            Pili, nisema wazi. Nilikusikia ukisema hakuna aliyeko juu ya sheria nchini. Hili si kweli. Rais yuko juu ya sheria; hata baadhi ya wateule wake wapo juu ya sheria. Rejea wale waliotuhumiwa, kwa mfano, kuguhshi vyeti vya kitaaluma na kuambiwa wachape mzigo. Je hawa hawako juu ya sheria? Wewe ni shahidi. Kama siyo, unaweza kueleza kuhusiana na mteule mwenzako mmoja aliyekutuhumu kuwa wewe na mwenzio Kamishina Susan Kaganda mlipewa rushwa ya shilingi milioni 50 kila mwezi kuruhusu shisha liuzwe jijini kinyume cha sheria. Kama kweli hakuna ambao wako juu ya sheria, je mlimfanya nini kama si kuogopa kumgusa kwa vile anaonekana kuwa juu ya sheria?
            Tatu, kama kweli hakuna aliyeko juu ya sheria, je ile kesi ya makosa yaliyotokea chini ya pua yako ya kuvamiwa kwa kituo cha runinga cha Clouds uliifanyia nini zaidi ya kuiacha ife kimyakimya kwa kuwaogopa walioko juu ya sheria unaosema hawapo wakati unajua wapo? Je hili nalo linahitaji elimu ya sheria kulijua kuwa si watanzania wote wako juu ya sheria au uliyasema hayo kujiridhisha na kuhamasisha wenzako hasa walioko chini yako waguse wasioguswa waishie kutimliwa? Nadhani kuna haja ya wakubwa zetu kuwa wakweli kwa wananchi wetu.
            Nne, ningekuomba ueleze historia yako, ulizaliwa lini, wapi na uliosomea wapi na lini maana inaonekana siku hizi mamlaka zetu zimeishiwa mawazo kiasi cha kushindwa au kuogopa kuanika historia za wateule wao ili wale wanawaongoza lau wawajue au kuwachoma pale wanapogundua wameongopa au kughushi vyeti.  Tumeonya kuhusiana na ujinga na uhuni huu bila mafaniko. Huenda kuna namna wenye kupendelea ufichi huu wanavyonufaika ima kuwaficha watu wao au kutokana na kutojua athari zake kwa taifa. Kwani, inashangaza kuwa utaratibu huu ulioanzishwa wakati wa awamu iliyopita baada ya kuhofia kueleza ukweli wa maisha ya wateule wengine wakiwa wa hovyo, kama huyu aliyekutuhumu, serikali ya sasa imeurithi na kuuendeleza. Sijui kama rais Magufuli anajua madhara ya mchezo huu mchafu ambao watendaji wake wameurithi toka tawala mbovu na za hovyo zilizopita zilizouanzisha kufichia maovu yake. Sidhani kama Magufuli anahitaji uoza huu tokana na uzalendo na uwazi wake. Je kinafichwa nini wakati wahusika ni watumishi wa umma unaopaswa kuujua nao wakaujua? Mbona zama za awamu ya kwanza na ya pili, hata kidogo ya tatu, kila mteule alielezwa historia yake vizuri ili wale anaowangoza wamjue vilivyo? Japo hili si kosa lako, nakuomba uvunje mwiko huu wa ambao umegeuka uchochoro wa kufichia uovu na umma kulipa viongozi na maafisa wasiofaa wengine wakiwa wametenda hata makosa ya jinai. Itisha mkutano na waandishi wa habari ufanye nao mahojiano maalum ili unaowangoza wakujue vizuri.
            Mbali na hayo hapo juu, nimefurahishwa na maazimio yako; kama utaweza kuyatekeleza vilivyo. Kwani ulikaririwa ukisema “nimeingia nikiwa msafi nataka nifanye kazi na kutoka hivi hivi, ninasikitika sana matukio makubwa ya mauaji na ujambazi yanatokea halafu polisi tunakuwa na kauli mbili. Kwa nini?” Hili azimio linatia imani ingawa usafi unaoongelea unatiwa doa na madai tuliyogusia hapo juu yaliyotolewa na mteule mwenzako asiyeguswa jambo ambalo si aibu kwa anayemkingia kifua bali nchi nzima. Uliongeza kuwa “nataka tufanye kazi kwa maslahi ya taifa. Tufanye kazi kwa maslahi ya wananchi kwani wao ndiyo mtaji wetu.” Hili nalo ni azimio safi sana kama utafanikiwa kulitekeleza vilivyo na kuhakikisha kila mmoja wa walio chini yako analitekeleza vilivyo.
            Naomba nichukue fursa hii kukupongeza kwa kuanza kazi na kasi inayofurahisha hasa baada ya kupangua kitengo kinachoshughulikia Udanganyifu au Fraud na kuagiza askari waache kuwapiga waandishi wa habari. Ningeomba uende mbele zaidi na kuwafundisha askari wako iwe marufuku kwao kuwapiga si waandishi wa habari tu bali wananchi wote kwa ujumla.kwani hawa ndiyo waajiri wao. Bila kodi yao wala mahitaji yao hakuna polisi anayehitajiwa. Wanapaswa kujua hili na kulisimamia, kulifanyia kazi na kulishika kikamilifu.
            Namalizia kwa kukutaka uzingatie ushauri niliotoa huku ukitekeleza au kutolea maelezo yale ambayo hayaeleweki lau unaowangoza tukujua na kuwa na imani nawe ukiachia mbali kukupa usaidizi katika kazi hii kubwa na ngumu ambayo imeangusha wengi hasa kuhusiana na haki za binadamu na namna ambavyo jeshi lako limekuwa likizivunja kwa kuwaonea wananchi wasio na hatia au wanasiasa, kukithiri kwa tuhuma za rushwa dhidi ya jeshi, ufisadi na usalama wa raia na mali zao. Nakutakia kila la heri katika nafasi yako mpya. Na Mungu akutangulie na kukuwezesha kufanikiwa. Na iwe hivyo.
Chanzo: Tanzania Daime Jumatano leo.

No comments: