The Chant of Savant

Tuesday 1 August 2017

Barua ya wazi kwa rais Magufuli


            Mheshimiwa rais John Pombe Magufuli,
Salamu sana na pongezi kwa kazi pevu yakusafisha nchi unayoifanya kiasi cha kuiletea Tanzania sifa kila uchao. Ama kweli nchi yetu, licha ya kugeuzwa shamba la bibi, ilikuwa inaelekea kubaya ambapo kila mapapa ya kiuchumi yalizoea kujiibia kama vile haina mwenyewe.
            Leo nina masuala machache tu kuhusiana na ulimbikizaji wa vyeo ambayo, kwa heshima na taadhima, naomba kuyaeleekeza kwako kama ushauri na namna ya kuonyesha hisia zangukama raia na shabiki wako.
            Kwa hesima naomba nijielekeze kwenye yafuatayo:
            Mosi, niliwahi kukusikia ukisema kuwa hutaruhusu watu kujilimbizia nyadhifa kama ilivyokuwa imejengeka na kuzoeleka kwa muda mrefu nchini ambapo watu wachache walijilimbikizia nyadhifa kana kwamba hakuna watanzania wengine wenye uwezo wa kushika nyadhifa hizo. Nashukuru kuwa, chini ya utawala wako, umeliona hili; na kuahidi kulifanyia kazi. Kimsingi, kujlimbikizia nyadhifa ilikuwa ni sehemu ma sura mojawapo ya ufisadi na uoza wa kimfumo. Kwani, kufanya hivyo kunawanyima wengine fursa. Huu ni ukweli usiopingika; na jambo la kimapinduzi lenye kulenga kuondosha ukiritimba wa madaraka kwenye ofisi za umma uliokuwa ukifanywa na kundi dogo la walaji wakubwa. Pia ni mapinduzi ya hali ya juu kwenye nchi ambako vyeo vinono vilibinafsishwa kwa familia za vigogo wachache chamani na serikalini hata mashirika ya umma.
            Pamoja na kukupongeza kwa uamuzi huu wenye tija kwa watanzania, nimegundua mapungufu kwenye azma yako. Hivyo, nachukuka fursa hii kukufichulia hii mianya na kutoa ushauri hasa nikizingatia kuwa wewe, kama binadamu yeyote mwenye mapungufu, huwezi kuyaona yote. Kwanza, naomba ninukuu maneno ya kada wa siku nyingi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Stephen Mashishanga aliyewahi kukaririwa akisema “Magufuli ni kiongozi mzuri sana, lakini sio malaika. Anayo mapungufu madogo madogo.” Huu ni ushahidi kuwa wewe si malaika asiyekosea wala mwenye kuweza kujua yote. Kwa kunukuu usemi huu, naomba nijielekeze kwenye haya mapungufu madogo madogo ambayo madhara yake yanaweza kuwa makubwa kwa taifa kama ilivyokuwa kiasi cha kuharibu dhamira yako safi. Nadhani, huenda, ni kutokana na mapungufu haya, mheshimiwa rais umesahau kuongoza kwa mfano katika baadhi ya mambo. Kwa mfano, wewe ni mwenyekiti wa CCM na rais wa Tanzania. Hivi, ni vyeo viwili tofauti tena vikubwa vinavyopaswa kushikiliwa na watu wawili tofauti kama tutazingatia azma yako ya kuondoa ukiritimba wa vyeo. Kwa maana nyingine ni kwamba una vyeo viwili jambo linalokinzana na azma na dhamira yako ya kuondoa ukiritimba wav yeo. Wahenga waliasa kuwa hisani huanzia nyumbani; na ukitaka kunihukumu mimi anza kujihukumu mwenyewe. Hilo moja.
            Pili, katika kupiga darubini yangu kuhusiana na wachache kujilimbikizia vyeo, nimegundua kuwa si wewe pekee mwenye kushikilia nyadhifa zaidi ya moja. Hata mawaziri wako ni wabunge na hapo hapo mawaziri. Je huoni kuwa nafasi walizoshikilia zingeweza kushikiliwa na watu wawili tofauti? Je hapa lengo na tamko lako la kuhakikisha hakuna anayejilimbikizia vyeo lilimaanisha baadhi ya watu au watanzania wote? Sheria siku zote ni kama msumeno. Naamini kama tungekuwa na sheria inayotamka kuwa hakuna anayeruhusiwa kushika nyadhifa zaidi ya moja, wala usingesahau ukashika nyadhifa mbili pamoja na mawaziri wako.
            Ukiachia mbali suala la mawaziri wako kuwa na nyadhifa zaidi ya moja, ulimteua rais mstaafu Jakaya Kikwete kuwa mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam (UDSM) wakati ukijua ni mstaafu anayelipwa marupurupu ya ustawi. Huoni kufanya hivyo, kumewazibia riziki wengine au ni kwa vile Kikwete ni mkubwa mwenzio. Hivyo, haguswi na amri yako?
            Mbali na Kikwete, umeendelea kuteua baadhi ya wastaafu kuwa ima wakuu wa wilaya au mikoa. Rejea wanajeshi wastaafu wanaolipwa mafao ya kustaafu na mishahara ya ukuu wa mikoa uliowateua kwenye baadhi ya mikoa. Rejea baadhi ya wakuu wa wilaya ambao ni wanajeshi ambao bado wako jeshini uliowateua kuwa wakuu wa wilaya. Je huoni kuwa hawa wana kipato zaidi ya kimoja au umesimamisha kimojawapo?
            Kwenye hili la kuwateua wanajeshi naona kama kuna kukiuka mhimili mmojawapo wa katiba ambayo inasema wazi kuwa watumishi wa umma na wa vyombo vya usalama hawapaswi kuwa na ushabiki kisiasa. Je unapomteua mwanajeshi kufanya kazi ya kiraia ya kisiasa huoni kama ni kuvunja katiba wazi wazi.
            Mheshimiwa rais nikukumbushe. Hapo mwaka 2010 mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Yusuf Asukile, aliyekuwa akiwania ubunge wa jimbo la Rungwe Magharibi, alikataliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kwa sababu alikuwa bado ni mtumishi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ); na baada ya hapo jeshi lilikuwa likimtafuta kumshughulikia kwa kuvunja sheria. Kanuni za Majeshi ya Ulinzi kwani, Sheria nambari nne (4) ya mabadiliko ya nane (8) katika Katiba ya Nchi ya mwaka 1992 ibara ya 147(3), mwanajeshi yeyote hatakiwikujihusisha katika masuala ya kisiasa.
 Je hawa wanaoteuliwa mbona hawakataliwi au ni kwa vile si wapinzani?
            Kwa hesima na taadhima; na kutokana na kujua una shughuli nyingi, naomba niishie barua yangu hapa; kwa kukuomba utupie macho mapungufu haya ambao yanaanzia nyumbani mwako.
Asante sana mheshimiwa rais.
Chanzo: Tanzania Daima J'tano kesho.

No comments: