The Chant of Savant

Sunday 6 August 2017

Magufuli ajifunze toka kwa Nkrumah na Nyerere

Image result for photos of magufuli
            Hakuna ubishi kuwa rais John Magufuli anakubalika si Tanzania tu bali duniani kote. Hii ni kutokana na jitihada zake za kupambana na maovu hasa ufisadi na matumizi mabaya ya fedha na raslimali za umma. Pamoja na uzuri huu, kuna upande mwingine ambao si mzuri kwa Magufuli mwenyewe hasa ikizingatiwa kuwa kazi anayofanya haiwapendezi wengi waliozoea kugeuza taifa shamba la bibi kama ambavyo rais amekuwa akilalamika mara kwa mara.
Magufuli amejizolea sifa nyingi mojawapo zikiwa ukweli, uwazi na kutoogopa kitu. Ndiyo maana amekuwa akiwaambia watanzania hatari na ugumu wa kazi ambayo anaifanya. Kwa kuzingatia hofu aliyo nayo rais na hatari na ugumu wa kazi yake, leo tungependa kumpa ushauri juu ya mambo anayopaswa kuepuka ili kuweza kufanikisha azma na kazi yake. Kwa mfano, rais Magufuli anasema mambo mengi ambayo hapaswi kuyasema kwa sababu za usalama zaidi ya kuyafanya siri na kuyaweka moyoni huku akiyafanyia kazi. Japo Magufuli ni mtaalamu wa fizikia, anapaswa kusoma historia ya Tanzania na Afrika kwa ujumla juu ya wale waliomtangulia wakifanya kama aliyofanya wengi wao wakakatizwa na maadui zao kirahisi. Katika kusoma historia kama si yeye basi wasaidizi na washauri wake ni kutaka kujifunza namna wazalendo wa Afrika waliomtangulia ima walivyoshinda au kushindwa vita yao.
            Mfano, viongozi magwiji wa ukombozi kama vile marais Kwame Nkrumah (Ghana), Patrice Lumumba (Kongo) hata Thomas Sankara (Burkina Faso) waliponzwa na ndimi zao. Waliweka wazi mipango yao dhidi ya mataifa kandamizi ya Ulaya kiasi cha kuwa rahisi ima kuwapindua au kuwaua. Mambo mengine anayosema ni classified yasiyopaswa kuweka hadharani. Hata anapoongelea namna watangulizi wake–ambao ameamua kuwalinda akidhani anawaridhisha–waliiuza nje kwa maslahi binafsi, ajue wao ni binadamu wanaoweza kumwonyesha sura tofauti na kile kilichoko moyoni. Wengi hawafurahii anayosema hasa yanayowaonyesha kama mafisadi walioingiza nchi kwenye matatizo.
            Kama atashindwa kusoma historia za magwiji waliotajwa hapo juu, basi asome historia ya marehemu Edward Sokoine waziri mkuu wa zamani wa Tanzania aliyeponzwa na uzalendo wake. Mbali na Sokoine, Magufuli anaweza kujifunza toka kwa marehemu baba wa taifa Mwl Julius Nyerere ambaye alipenda sana kuwakosoa wazungu bila kuonyesha wazi chuki yake wala kuwambia mipango yao dhidi yao. Mfano mwingine ni wa Sankara aliyeponzwa na kuwaambia ukweli wazungu ukiachia mbali kuleta mapinduzi ya kifikra na kiutendaji barani Afrika kwa kuifanya nchi yake kujitegemea kwa mambo mengi kwa muda mfupi aliokaa madarakani.  Japo Magufuli amesema kuwa lazima awaambie watanzania ukweli, hapaswi kusema kila kitu hasa kile kinachoweza kuhatarisha usalama wake. Mfano, Magufuli ajue hawa wawekezaji aliowakaba koo kiasi cha kuamua kukubali kushiriki majadiliano, hawaridhishwi wala kuzipenda hatua anazochukua kuwanyang’anya tonge mdomoni hasa ikizingatiwa kuwa wengi wamezoea kufanya hivyo kwa miaka mingi tu kiasi cha kuona jinai hii kama hai yao kisheria. Anapaswa kujua kuwa wanaweza kumchekea ili wampate baadaye. Nani mara hii amesahau namna marehemu Hugo Chavez, rais wa zamani wa Venezuela alivyoichachafya Marekani na wanyonyaji wa kimataifa wakaishia kumuambukiza kansa?
            Ukiachia mbali mifano hapo juu, Magufuli anapaswa kujiuliza ni kwanini Acacia waliwahi kutishia kwenda kushitaki Tanzania kwenye mahakama ya kimataifa kabla hawajabadili mwelekeo na kukubali kushiriki mazungumzo. Hawa wachukuaji hawaji kwa furaha kama wanavyoonyesha kwenye nyuso zao. Wanacheka usoni; lakini rohoni wanalia wakitamani wampate mbaya wao ambaye ni Magufuli. Pia Magufuli anapaswa kufahamu kuwa hata wale waliowawezesha wawekezaji wezi hawa hawafurahii kuona hatua zinazochukuliwa dhidi yao. Magufuli ameonekana kuwa mwiba si kwa wawekezaji tu bali hata waliomtangulia.
            Mfano alipokuwa akihutubia kule Manyoni Mkoani Singida alikemea vitendo na uoza vilivyokuwa vikifanyika serikalini kabla ya kuingia madarakani. Alisema kuwa serikalini ilikuwa ni utumbuaji wa mali za maskini ambap wengi waliwekeza kwenye safari za Ulaya na semina na madhambi mengine. Kwa kukemea uzururaji, Magufuli alikuwa akinmanga Jakaye Kikwete aliyesifika kwa kuzunguka dunia akiandamana na marafiki zake na walaji wengine walioigeuza nchi kuwa chaka la uhalifu.
            Hakuna suala lililowaacha uchi watangulizi wake kama pale Magufuli alipoongelea kuhusiana na ukosefu wa madawati mashuleni ambapo serikali zilizomtangulia zilikuwa hazitoi umuhimu wowote suala la elimu hasa mazingira rafiki kielimu kwa watoto wa kitanzania. Mbali na elimu, Magufuli aliongelea uwepo wa wafanyakazi hewa wapatao 19,000 ambao serikali zilizomtangulia liliacha wahujumu taifa. Aliwalinganisha na nyoka akimaanisha kuwa wale waliowafuga walikuwa wafuga nyoka na adui wakubwa wa watanzania hasa maskini. Magufuli alisema kuwa ni Tanzania tu ambapo wafanyakazi hewa wengi kiasi hiki wangeachiwa kuendelea kuibia umma huku viongozi wakipoteza fedha na muda kwenye uzururaji.
            Hakuna jambo baya kama kueleza ukweli kwa mtu au watu wasiokuwa wakweli.  Japo anayosema Magufuli ni ukweli, wenzake hawaoni huu ukweli tokana na ukweli kuwa waliyofanya yanawaumbua japo hawataki kuukubali ukweli.
            Tumalizie kwa kumuasa rais afahamu kuwa hawezi kujua yote. Na tunafanya hivi kwa upendo kwake na kwa taifa hasa kipindi hiki cha mageuzi na mpito kinachopaswa kuwa cha kujenga umakini wa hali ya juu ili kufanikiwa. Tuko nyuma yako na tunakuunga mkono mheshimiwa rais. Na tungeomba na kutaka mapambano yako yafanikiwe kwa faida yetu na vizazi vijavyo.  Hatuna cha kukulipa kwa namna ulivyojitoa mhanga kwa ajili ya taifa letu ukiwa ni somo kubwa na tosha kwa Afrika.
Chanzo: Tanzania Daima J'pili leo.

No comments: