The Chant of Savant

Friday 11 August 2017

Mlevi apanga kuanzisha chuo kikuu MUST













Image result for photos of paul makondaPichani ni Smuel Chitalilo (Bingwa wa kughushi), Victor Mwambalaswa, Emanuel Nchimbi, Raphael Chegeni,Makongoro Mahanga,Mary Nagu, William Lukuvi, Diodurus Kamala na Paul Makonda.
            Baada ya kuona vyoo vikuu vinaota kama uyoga huku vingi vikiwa havina ithibati wala nia njema zaidi ya kutegeneza njuluku na kuijaza jamii ujinga na vihiyo, mlevi anapanga kuanzisha chuo kikuu cha Mlevi University of Science and Technology (MUST). Hii ni baada ya kufanya utafiti kwa muda mrefu na kugundua kuwa kumbe utapeli unalipa hasa kwenye kaya za walevi wanaopenda dezo bila kuvuja jasho. Mwanzoni nilipanga kuanzisha dhehebu la dini ili niwaibie wajinga na wale wote walioharibika na kuharibikiwa kiasi cha kutegemea kuboresha maisha yao kupitia miujiza wasijue miujiza wanayotangaziwa si chochote bali kuwatajirisha na kuwaneemesha wachache. Kwa vile naamini katika kufa, nilistuka nisije kukutana na Bwana God siku moja akanichoma motoni milele. Naona yule anatikisa kichwa akidhani nasukumwa na bangi na ulabu. Kwani huwaoni mabilionea walioibuka hadi kununua mapipa bila kutaja vyanzo vya ukwasi wao kutokana na kutokuwa na sheria ya kuwabana waeleze walivyochuma ukwasi huu?
            Tukiachana na matapeli wa kiroho waliojaa roho mtakakitu wakijifanya wana roho mtakatifu, mwenzenu napanga kuanzisha chuo lau niwapate wanene walioghushi kama vile akina Bashute. Najua hapa nitavuna kweli kweli hasa ikizingatiwa kuwa wanene hawa huwa hawataki kupata taabu ya kuumiza vichwa kusotea shahada. Mara hii mmewasahau wale vihiyo aliowatolea uvivu mwanaharakati Keinerugaba Msematruth? Wako wapi waliotishia kumpeleka kwa pilato zaidi ya kunywea kama mbwa walioiba mafuta? Hawa nao nawakaribisha waje kwangu niwape zana waonekane wasomi hata kama ni vihiyo wa kawaida wanaopaswa kuuza nyanya au kufagia barabara lakini siyo kutanua kwenye ofisi za umma za walevi. Msidhani natania? Shauri yenu; I am dead serious, especially at this time the exercise of auditing academic certificates has butchered to save the son of dingi Bashute.
             Kwa wale watakaovutiwa na michongo yangu wanachopaswa kufanya ni kuja na kujiorodhesha na kwenda zao home. Mie baada ya muda mfupi nawapa shahada yoyote wanazotaka. Isitoshe mie nina nafuu ikilinganishwa na matapeli wengine kama wale niliowahi kuwananga na kuwaanika waliokuwa wakitoa PhDs hata kwa mamantilie wakidai wamefanya jambo fulani la maana kwa jamii. Kwanini kwangu ni muhimu na salama? Mie nachotafuta ni njuluku wala si uroda na upuuzi mwingine kama wale wanaotoa shahada za pupi aka nguo ya inside. Hakuna shahada ya gagulo kwangu. Unaleta mchicha, unaondoka na bonge la shahada ambalo linaheshimika hata majuu. Wala hakuna hata haja ya kwenda majuu kuvunga unakwenda kufanya masters wala PhD.
            Mbali na kutaka kuwatoa uchache wanene vihiyo, nimepanga kuanzisha chuo ili kufichia fedha zangu za bwimbwi au tuseme kutakatisha bila kusumbuliwa na mkono wa sheria wala akina Takokuru wanaosifika nao wa kupiga huku wakijfanya wanazuia rushua. Hamkumsikia yule mhasibu aliyekutikana ana mabilioni bila maelezo? Kwa vile kaya hii mlevi haulizwi kafanya nini hadi kuwa bilionea, nitashindwa nini kununua dege la bei mbaya kama lile la Trump alilonunua yule mchunaji tata anayehubiri siasa badala ya neno la God ukiachia mbali kupoteza muda mwingi akihubiri maovu ya Bashite badala ya kueneza neno. Huyu naye nitampiga. Kwani amekuwa akijiita daktari bila kueleza alivyopata udaktari wake. Ili kumnasa kisawa sawa, nitawapa njuluku waandishi wa umbea ili wamfichue aweze kuja kwangu nami nimuonyeshe miujiza kama anayodai kuwaonyesha wajinga wengi wanaomwamini na kumwabudia wasijue ni msanii kama yule mama aliyejipachika uchunaji na udaktari. Hivi naye hekalu lake alilootesha kwenye sehemu isiyoruhusiwa limeishia wapi? Maana, baada ya juzi kudeku picha za mahekalu ya profedheha Jay sikuona lake kwenye orodha au dingi hajamdeku?
            Kwa wepenzi wa siasa; na wanaotaka kugombea ulaji wa kisiasa kayani, wawahi haraka. Kwani nina mpango wa kutoa shahada za juu kwenye sekta kama vile Winning  Political Strategies, How To Lure Voters na nyingine nyingi kama vile Political Psychology Analysis na Electoral Fraud Mastery in Shake Democracy ambayo juzi juzi nilitoa kwa jamaa mmoja toka kaya ya jirani akaenda kuukwaa ulaji kwa kucheza na makompyuta.
            Mbali na shahada za siasa, nina mpango wa kutoa shahada za Biashara, Ndoa, Bahati, Ujanja hata namna ya kukwepa mkono wa sheria. Hivyo, akina Rwetumbuliwa, Singasinga na Manjiii, wawahi au kutuma wawakilishi wao niwatoe lupango.
Kwa vile sijapata kanywaji, leo naachia hapa nikienda kutafakari mishemishe nyingine za kuwakomboa vihiyo na walevi apeche alolo.
Chanzo: Nipashe J'mosi kesho.

No comments: