The Chant of Savant

Wednesday 20 September 2017

Kijjiwe kwenda Nairobi kumjulia hali Lissu

        
            Baada ya mwenzetu kufanyiwa kitu mbaya na mahabithi wanaoitwa watu wasiojulikana wakati wanajulikana, tuna mpango wa kutuma wajumbe kwenda kumjulia hali kama mchango wetu na kuunga mkono jitihada zake za kupigania haki za wachovu.
            Kapende anaingia akiwa na gazeti lenye picha ya Tunduni Lissu.  Anatusomea kichwa cha habari “sasa Tunduni anaanza kupata nafuu na wanaomtakia mabaya yawapate wao na wake zao au waume zao na watoto familia ndugu jamaa na marafiki zao huku yakiwaacha maadui zao.” Hata kabla ya kuendelea anatokwa jasho huku akihema utadhani katoka kwenye nyumba inayoungua moto.
            Kabla ya kuendelea Msomi Mkatatamaa anaamua kuingilia kati huku akitabasamu na kuhoji “mheshimiwa Kapende hebu nipige darasa la bure. Kweli hicho ni kichwa cha habari au ni kichwa chako? Maana sijawahi kuona kichwa cha habari kama hicho.”
            Kapende anatabasamu na kuzoza “Msomi umeninasa.  Ni kichwa cha habari. Sema nimeongeza na yangu ya kichwani. Hivyo, unaweza kusema ni vichwa vya habari. Lakini hata hivyo si ujumbe umefika kuwa nina maya na wanahizaya na wajalaana waliommiminia shaba shujaa yetu?”
            Mgoshi Machungi anachomekea “hata ingekuwa mimi tingeongeza. Maana hii kitu aiyofanyiwa huyu shujaa inanifanya nitamani kumpiga mtu zongo. Hivi hii kaya inakwenda wapi; au tiseme inapeekeshwa wapi wagoshi? Maana tangu shujaa afanyiwe huu unyama, siikai haionyeshi kustuka waa kutaka kutoa maeezo ii tiandastandi na kuchangia kibidi. Je kunani nyuma ya pazia au kwa vie Tundi Issu ni mpingaji?”
            Mjjinga anakamua mic “Mgoshi jibu unalo. Unadhani angekuwa mwishiwa wa chama twawala hawa wasiojulikana, japo wanajulikana, wangekuwa bado mitaani wakitanua na kula walichopewa kufanya unyama huu ambao siku moja utaumbua hata wale ambao hukutegemea?  Huoni hata watajwa kwenye ujambazi wa almas akina Andru Chenga na Bill Ngereza bado wanaengwaengwa badala ya kuonyeshwa mlango. Heri watu wasiojulikana, wangekuwa wazalendo, wangehangaishwa na hawa mafisadi wakubwa na wenye roho mbay. We acha tu. Nina hasira kiasi kwamba nikipata hawa wasiojulikana naweza kuwabaka hadharani, sorry, kuwafanyia kitu mbaya ili wakawaambie mama zao na wake zao kama wao warume kweli.”
            Bi Sofia Lion aka Kanungaembe anaamua kumpinga Mijjinga “kaka sasa unakwenda kubaya. Unadhani kuwanonihino ni suluhu au msaada kwa mhanga? Nadhani tuwabane wahusika wawataje hawa wanaowajua na kuwaita watu wasiojulikana. Sasa kama wahalifu kama hawa tena wajinga, washamba, na wapumbavu wanaweza kufanya unyama wasijulikane, hao wenye mamlaka wanatawala nini? Je wao ni salama? Au wanangoja yawafike kama si wao watu wao. Ukipanda mbigiri, utavuna mbigiri si maua.”
            Mpemba anaamua kula mic “Yakhe acha da Sofia nami nkuchomekee ashakum si matusi; nadhani wanipata.  Kama yupo awezaye kuwapata hawa watu wasiojulikana waniotaka ua wenzao, dawa yao ni kuwaua vivo hivo walivotaka kunnua Tunduni.  Hapa lazima niseme ukweli lazima tufanya haq bin haq. Untoboa mato nkutoboa mato; hiyo ndiyo haki.”
            Kanji anaamua kutia guu “mimi dugu yangu hapana taka shari vala vunja seria. Lakini kama nafikiri juu ya hii vatu vasivojulikana nafanyia Tunduni, kama napata yeye nafanya kitu baya hata kama baka yeye dugu zanguni hapana sikia baya bali raha. Sasa kama navwanga risasi mingi kama naua jini sisi fanya nini? Kama natoboa roho ya Tunduni, vapi baya toboa yeye.”
            Kijiwe hakina mbavu hadi da Sofia mshirika wa Kanji anaziba uso huku akiangua kicheko tokana na Kanji anavyobukanya uswa na kutishia kumwaga radhi.
            Mbwa Mwitu anauliza huku akicheka “Kanji veve iko taka toboa nani na vapi na kvanini dugu yangu kama iko fuata seria?”
            Kanji hajivungi; anajibu ‘Kama Tunduni iko dugu yako va damu navezasema hii neno nasema sasa au tafuta hii vatu vasivojulikana na kufanya kitu baya navo iumie kama Tunduni naumia yeye na family yake?’
            Mheshimiwa Bwege aliyekuwa kimya akiangalia anaamua kutia guu “wakati mwingine kijiwe hiki kinashangaza. Kila anayeongea anatamani. Kwanini msifanye kweli; kama noma na iwe noma? Kila anayeongea anatamani kuwafanyia kitu mbaya hawa malaya wa kisiasa. Mara natamani niwabake; mara niwafanyie kitu mbaya; mara hiki; mara kile. Sasa mimi nasema. Hivi kuua na kubaka ni lipi kosa kubwa zaidi?  Basi kuanzia leo nasema wanakijiwe kuondoa dada yangu Sofia, tuwatafute hawa wahalifu tuwabane ili waweze kuonea aibu ubakaji wa kaya wanaotaka kuutekeleza kwa kutaka kuua watu wasio na hatia. Hapa hakuna kuwaangalia nyani usoni. Hii kaya ni yetu wala siyo  ya mama zao.”
            Kiiwe kikiwa kinanoga si likapita gari jeupe aina ya Nissan! Kama siyo mwenye gari hili kujiwahi na kutoka nje na kusema yeye tumtazame na anajulikana, huenda tungemnyotoa roho tusijue kuwa kumbe ndata walikosea kusakanya ndinga zote zenye rangi sawa na lile la watu wasiojulikana. Sijui kwanini hawakutaka kulifuatilia kwa namba walizopewa na wahanga!
Chanzo: Tanzania Daima, J'tano leo.

No comments: