The Chant of Savant

Saturday 14 October 2017

Mlevi amkumbuka mzee Mchonga Nyerere


          Baba Mwl JKN Mchonga, shikamoo,
            Japo umelala kwenye pumziko la milele, naamini unaniona na kunisikia. Kama hutanisikia, wengine watanisikia.  Hivyo, sina shaka utasoma hii kitu ambayo nakuandikia wakati nikikumbuka mwaka wa 18 tangu ututoke kwa masikitiko makubwa.  Habari za huko? Je ulishaonana na akina Nelson Mandela, Sir Ketumile Masire na kijana wako John Garang de Mabior yule wa Sudan uliyemsaidia akasomea kule Lushoto? Basi baba, alifariki kwenye ajali ya kutatanisha akitokea kwa  M7. Kifo chake kilisababisha kifo cha Sudan. Kwani Sudan uliyoacha moja sasa imegawanyika kati ya Kaskazini na Kusini, Waafrika na Waarabu feki, Wakristo na Waislam bila kusahau Darfur na Nuba Mountains  ambazo nazo ziko matatani zikipanga kutengana na Sudan ya Kaskazini inayobagua waswahili wazi wazi wakati nao ni waswahili wanaoongea kimanga tu kinachowalewesha kiasi cha kujihisi wao si waswahili bali wamanga.
            Baba, je una habari yule kijana wako mwingine uliyemsaidia kule kwa Nduli Yoweri M7 bado yuko madarakani huku akiwa kwenye harakati za kubadili katiba ili aendelee kuwahenyesha walevi wa UG? Anataka kugeuka Kamuzu Banda wa kizazi hiki. Basi baba, siku hizi kubadili katiba ili kubakia madarakani imegeuka fasheni. Burundi na Rwanda walishabadili zao. Kama nilivyosema, UG ndiyo hiyo iko mbioni. Hapa kwetu bado. Wapo wapuuzi fulani walifikia hata kupeleka mswaada Mjengoni wakitaka ukomo wa urahis uondolewe.  Baba, tena kabla sijasahau, una habari kuwa kwa sasa tuna rahis mpya aitwaye Joni Kanywaji Magu? Kijana huyu ni madhubuti sana pamoja na udhaifu kidogo. Kwani, tangu aingie pale Patakatifu pa Patakatifu, ameanza kuisafisha kaya kiasi cha mafisadi mapapa kuanza kunonihino kwenye debe.  Kijana amerejesha heshima ya kaya si haba. Kwani ninapokuandikia, Muhimbili kuna vitanda vya kutosha. Shule zote za Msingi zina madawati. Jamaa amebana matumizi.  Hataki kuzurura kama yale mabalaa mawili moja ulilopiga tafu na jingine ulilopiga chini  yalivyokuwa yakizurura huku yakiongozana na misururu ya walaji.
            Tena kabla ya kusahau, mama Maria siku hizi anazeeka kiasi cha kushindwa kuhudhuria baadhi ya sherehe. Hata hivyo, bado wamo si haba pamoja na umri kushuhudia. Naona unatikisa kichwa. Usifanye wivu hasa ikizingatiwa kuwa huyu ni bibi yangu. Hayo ya wajukuu tuyaache.
            Mwalimu, sasa niruhusu kwa heshima nikupe salama za walevi wako wa justice. Wanakumiss ile mbaya. Hakuna siku inayopita bila kukumbuka. Mwalimu, huwezi kuamini kuwa umaarufu wako unapanda kwa kasi kiasi cha kuwapita wengi wa walio hai hasa wale waliobomoa mema yako yote uliyoanzisha tokana na ima ubinafsi, ujinga au upogo. Hapa ninapoandika, wengine wanalindwa na kifua cha munene. Vinginevyo, wangekuwa wakinonihino kule Keko kama siyo Segerea.
            Mwalimu, good news ni kwamba yale madini uliyokuwa umegoma kuchimba wakaja wakora wakayachimba na kuyagawa kama peremende sasa yanaanza kuwafaa walevi. Haka ka kijana ka Joni kameamua kufumua mikataba yote ya kipuuzi ili lau walevi tunufaike na mawe yetu kama ulivyoona mbali. Basi Mwalimu, baada ya kajamaa kutia timu ikulu si kalianzisha mchakato wa kufumua mikataba yote. Wengi wa waliofanya upuuzi huu wanaishi tumbo moto wasijue nini kitawatokea kesho yake.
            Je unakumbuka ile kashfa ya IpTL? Yule nshomile na gabacholi waliojiona kuwa serikali ndani ya serikali sasa wanaozea korokoroni baada ya Ka-Joni kuamua wapewe haki yao. Siku hizi kuna heshima kama zama za utawala wako. Mafisadi hawatukogi kama ilivyokuwa baadaye.
             Mwalimu, unaweza kuamini kuwa siku hizi kugeuza ofisi za umma nyenzo ya kuombea rushwa na kupiga domo ni historia?  Mambo yamebadilika. Hata wale walioghushi sifa za kitaaluma, japo si wote kutokana na baadhi wachache kukikingiwa kifua, wanalia na kusaga meno. Hata hivyo, zoezi hili lilikufa ghafla baada ya kitoto kimoja chenye kujikomba kwa munene kubainika kilighushi vyeti, hivyo, kufanya akikingie kifua na kuamua kuachana na kuwasaka vilaza na vihiyo wengine.
            Mwalimu, miaka 18 si haba. Tangu uondoke mambo mengi yametokea mojawapo ikiwa ni kutimia kwa ndoto yako ya kuhamia Dodoma. Ninapoandika, wizara karibia zote zishahamia huko. Ngoja, nilitaka kusahau. Una habari kuwa siku hizi Dar  na Mwanza zina flyovers zile tulizokuwa tukizisikia Nairobi? To make things worse, kuna daraja la kuunganisha Feri na Kigamboni na linaitwa Nyerere.
            Kwa vile mhariri amenipa nafasi finyo, naomba Mwalimu niachie hapa kwa machache toka mjini niliyokujulisha. Muhimu, tunakupenda; tunakukumbuka na kukumisi kichizi na kinomi mwalimu.  Kwa leo ni hayo. Basi piga mbonji peponi milele mwalimu.
Chanzo; Nipashe J'mosi leo.

No comments: