The Chant of Savant

Tuesday 13 February 2018

Kijiwe chajadili ununga wa kisiasa kayani

          Baada ya kujikita kwenye uchafuzi wa maadili wiki iliyopita na kupata muitikio wa kuua mtu, Kijiwe leo kinarejea kujadili kadhia mojawapo ya uvunjaji maadili, yaani uvunjaji wa amri ya sita au tuseme kwa lugha rahisi unungaembe wa kisiasa ni aina fulani ya uchangudoa. Kwa wale wanaotoka etimolojia ya dhana nzima, unungaembe wa kisiasa ni kitendo cha mchovu kuwa na washikaji wengi. Simpo. Hata hivyo, leo tutaongelea uchangudoa tofauti na huu wa mwili. Tutaongelea uchangu wa kichwani aka wa kisiasa.
            Kapende anaingia akiwa na gazeti la Danganyika Daima. Anaamkua na kulibwa mezani. Mchunguliaji anajiwahi kama kawaida yake. Kapende anazoza “jamani mmeona wachovu wanavyobadili vyama kama daladala. Kunani jamani mbona mwenzenu nachanganyikiwa kiasi cha kushindwa kuelewa jinai hii ya kujitakia?”
            Mzee Meneno ambaye wiki jana hakuudhuria Ndevu anakula mic “unashangaa na kuulizia huu ununga wa kisiasa ambao unaendeshwa na njaa ya kukosa adabu na aibu! Nadhani kuna sababu nyingi nyuma ya uchangu huu wa kimaadili mojawapo ikiwa ni njaa hasa iliyopanda vichwani na kuendekezwa.”
            Kabla ya kuendelea Mpemba anamnyang’anya mic na kunena “yakhe uniosema ni ya kweli tupu.  Mie naona wengine wasukumwa na uchumia tumbo wala si njaa. Kwani wengi wanao ukwasi. Hawana njaa hata kidogo bali tamaa na kutaka vya dezo muda wote ukiachia mbali kuishiwa kulhali.”
            Msomi Mkatatamaa anaamua kutia guu “wasemaji mliotangulia mmenena vitu vya maana sana. Tangu siasa iwe dampo la kila anayetafuta ulaji bila kujali usomi wake unategemea nini? kuna wachovu ambao licha ya kuwa na elimu za kuungaunga au kughushi, hawana sifa yoyote ya kuajiriwa na kufanya chochote zaidi ya siasa ambayo kwa kaya za uswekeni ni ubingwa wa kupiga domo na usanii usiofuata kanuni yoyote. Hivyo, kwa wachovu kama hawa kubadilisha vyama kama nepi si jambo geni wala la kushangaza. Wana hasara gani iwapo wanapata tonge hata kwa kujivua nguo na kujidhalilisha kama tunavyoshuhudia? Kwangu, kinachoshangaza ni mfumo huu unaoruhusu huu uchangudoa wa kimaadili unaoanza kuzoeleka katika anga za ulaji wa dezo wa wachovu na raslimali zao.”
            Kabla ya kuendelea, Kanji anampoka mic “veve kumbusha mimi ile changu nasema eti napenda kuu balaa. Yaani baba jima napenda baba nyingine balaa? Sasa kama napenda baba nyingine balaa bibi yako tapenda wipi dugu yangu? Hata Bombei hapana sikia kufuru kama hii dugu yangu. Sasa kama baba napenda baba nyingine balaa nani tapenda mama na toto?”
            Mijjinga anampoka mic Kanji na kuzoza “hivi kama tutakuwa wakweli kwa nafsi zetu hii naayo ni sera ya kutangaza majukwaani? Kweli kuna mapenzi katika sanaa za ulaji ndugu zanguni? Ukisikia kufilisika kimaadili ndiyo huku. Jamaa mwenyewe alishasema hatafuti kupendwa bali kuwatumikia wachovu.”
            Kabla ya Mijjinga kuendelea kudana, Kapende anaamua kumtoa wasi wasi Kanji kwa kusema “Kanji wala huna cha kushangaa. Njaa inapopanda kichwani msaka tonge yoyote anaweza kufanya lolote hata kama ni kujivua nguo kama hili baba lililoropoka. Kimsingi, vyangu kama hawa wanafanya usanii ili tonge lipande kinywani. Hawana mapenzi yoyote na wale wanaowapenda zaidi ya kupenda ulaji wa dezo utokanao na usanii huu wa kisiasa. Hakuna zaidi ya hili ndugu yangu. Mimi nawajua nimeishi nao tangu nikifanya kazi ya kupiga picha. Kimsingi, kinachoendelea ni unungaembe wa kisiasa.”
            Kitendo cha kutaja unungaembe kinamuibia Da Sofia Lion aka Kanungaembe ambaye anaamua kula mic “kama ununga wa kisiasa umeruhusiwa hivi, kwanini kuwaandama dada poa wakati kaka poa wa kisiasa wakivumiliwa wakati hawamuuzi, kumtapeli wala kumuumiza mchovu yoyote? Maskini kutokana na ukapa uliotamalaki wanajiuzia miili yao sawa na hawa wasanii uchwara wanaouza roho za wenzao bila aibu wala huruma.”
            Mipawa anaamua kula mic “hapa dada Sofia umetia na kunena neno la maana.  Kimsingi, wasanii hawa njaa wanatiana aibu bila kufikiri wakidhani wachovu ni wajinga wasioweza kuambua utapeli huu Dhahiri. Itikadi ni imani na msimamo. Huwezi kudandia vyama kama dala dala ukabakia kuwa na maana.”
            “Nadhani wewe bado unaota zama za maadili za mzee Mchonga. Siku hizi siasa ni ulaji hata kama wa kula bila kunawa. Itikadi na msimamo vilikufa na mzee Mchonga kiasi cha maadili kugeuka madili. Hata hili linakushinda?” anachomekea Mbwamwitu huku akivuta kombe lake na kubwia kwa madaha.
            Mgoshi Machungi mwana wa Shikilango aliyekuwa akikamua kahawa yake anaamua kutia guu “sisi kue Ushoto huita haya mnayoshangaa mambeza yaani kufanya mambo kana kwamba anayefanya hivyo hana akii timamu kama yule kidhabu nabii Tito mjaana aiyekuwa akihimiza dini ya mashetani ya kutenda maovu. Nashukuu Mungu amekamatwa na kupigwa stop maa moja. Sijui tinapeekeshwa wapi jamani ambao kia mjaana anajifanyia atakavyo?”
            Kijiwe kikiwa kinanoga si akapita msanii aliyesema anampenda Mpayukaji balaa. Acha tumzonge lau tujue alichomaanisha ili ti-understand.
Chanzo: Tanzania Daima, Feb., 14, 2018.

No comments: